Siri moja wapo ya
kuwa tajiri ni kujenga tabia ya kuweka akiba. Kwa wajasiriamali wadogo swala la
kuweka pesa zao benki na kukopa huwa ni swala gumu hasa vijijini ambako hakuna
huduma hiyo, kuna njia nyingine ambayo wataalamu wamebuni kuwawezesha kuitumia
nayo ni kuweka akiba zao kwenye VICOBA. Watu wengi wamekuwa wakijiuliza
vicoba ni nini? Leo nitaelezea kuhusu historia ya mfumo wa VICOBA muundo,
kanuni na taratibu za mfumo wa kuweka na kukopa vijijini (Village
Community Banks - VICOBA)
Mfumo wa
Kuweka na Kukopa Vijijini (Village Community Banks - VICOBA) ni mpya hapa
nchini kwetu, mfumo huu uliingizwa nchini na Shirika la CARE International,
Tanzania mwaka 2000. VICOBA imeenea katika sehemu nyingi Tanzania na idadi ya
Wanachama wa VICOBA Tanzania inakadiriwa kuwa 25,542, hisa 25,542 zenye thamani
ya Tshs. 2,298,780,000 vikundi 912 wastani wa wanachama 28 kila kikundi.
Mikopo iliyotolewa ni Tshs. 3,065,040,000. Mfumo huu humilikiwa na wanachama
wenyewe kwa njia ya kujitolea, kujenga uwezo wa mtaji, kubuni miradi ya
kifamilia, kutumia vizuri mikopo. Mfumo huu ni rahisi kuendesha kwani unatumia
kumbu kumbu rahisi kwa mazingira ya wanachama. Huwawezesha wanachama
kuweka akiba na kukopeshana bila kuomba msaada kwa wafadhili wala kukopa benki.
Faida inayopatikana hugawiwa kwa wanachama kutokana na mchango wa kila
mwanachama. Mfumo wa VICOBA ni shirikishi unaojengwa katika msingi ya
upendo, ushirikiano na kuaminiana miongoni mwa wanachama. Kutokana na sharti
hili muhimu, mfumo huu unachangia kurekebisha watu wenye tabia mbaya na
wasiokubalika katika jamii na kuwafanya wawe raia wema, ili wakubalike kwenye
vikundi na kudhaminiwa na wenzao. Mfumo huu unalenga katika kubadilisha
taratibu mbaya (zisizoendelevu) za maisha ili kuziwezesha familia
kujiewekea malengo maalumu ya maisha na kuandaa na kuitekeleza mikakati
ya kuyafikia malengo yao hatua kwa hatua. Hii ni pamoja na kuwa na matumizi
mazuri ya fedha kutika familia, kujituma katika kufanya kazi. Mfumo huu unaurahisi wa kupata mikopo ya
masharti nafuu kijijini na husaidia kuwawezesha wanakijiji (wanachama)
kujiwekea hisa kila wiki katika benki yao katika eneo husika na kwa kiwango
kidogo kulingana na uwezo wao pasipo na gharama yoyote.
Huduma
zifuatazo hutolewa na Vicoba kama vile; uundaji wa Vikundi vya Kuweka na Kukopa
Vijijini (VICOBA) kibenki kwa kujitolea, kuandaa vifaa vya kibenki na masomo ya
kufundishia, kutoa mafunzo ya uongozi wa vikundi na kuweka na kukopa.
Kutoa mafunzo ya biashara yanayolenga katika kuwawezesha wanachama kuweza
kuchagua miradi mizuri ya kiuchumi,teknolojia nyepesi, kuandaa mipango mizuri
ya kuanzisha na kuendesha miradi yao na mbinu za kusimamaia miradi hiyo kwa
faida. Kufanya utafiti wa masoko na kuandaa mikakati ya masoko, Kuendesha
shughuli za kibenki na ushauri mkwa vikundi. Kusaidia vikundi kuratibu
usambazaji wa pembejeo na raslimali zingine.
Muundo wa uongozi
kikundi cha VICOBA huundwa na wajumbe tisa ambao huchaguliwa kidemokrasia kwa
kuzingatia kazi za kila kiongozi na uwezo walionao. Miongoni mwa viongozi hawa
ni: wajumbe watano wa Kamati Tendaji yaani Mwenyekiti, Katibu, Mweka Hazina, na
wahesabuji fedha wawili. Kundi la pili ni la viongozi wa kikundi ni: washika
funguo za sanduku la kikundi watatu na mtunza nidhamu wa kikundi. Viongozi hawa
huchaguliwa kidemokrasia na wanachama wote kwa kuzingatia sifa walizonazo
katika kuongoza kikundi. Viongozi hawa hubaki madarakani kwa mzunguko mmoja
ambapo sawa na miezi 9 - au zaidi Mzunguko wa kikundi hufungwa kwa muda wa wiki
moja (1) hadi tatu (3), mara nyingi hii, hufanywa wakati wa sherehe za kidini
au za mwisho wa mwaka au wakati wa kazi nyingi za kilimo, ukame, au uhaba
mkubwa wa chakula, maji nk. Hisa zote zinazopatikana hugawanywa kwa wanachama
pamoja na faida ili kusaidia kulipia gharama mbalimbali za familia kama vile
kilimo, kununua chakula, nguo, ada za shule za watoto, na kugharamia sherehe na
matumizi mengine muhimu ya familia. Mzunguko hufungwa ili kutoa nafasi ya
kutosha kwa wanachama kushiriki kikamilifu katika kutatua matatizo
yanayozikabili familia zao kipindi hicho. Mzunguko mpya huanza mara ya muda
uliopangwa kupumzika kwisha. Marekebisho mhimu ya sheria za kikundi, uongozi na
taratibu za kuendesha mikutano ni muhimu kufanyika wakati wa kufunga mzunguko
ili kuboresha ufanisi wa kikundi katika mzunguko unaofuata.
Shughuli zote za
vikundi vya VICOBA huendeshwa na wanavikundi wenyewe kwa njia ya kujitolea.
Uzoefu unaonyesha kuwa wanavikundi huweza kuendesha vizuri shughuli zao baada
ya kupatiwa mafunzo haya ya uongozi na usimamizi wa kazi za vikundi kutoka kwa
wataalamu wa mfumo wa VICOBA. Kazi/wajibu wa wanakikundi ni: - Kushiriki kwenye
mikutano na mafunzo ya vikundi. - Kuweka hisa za kila wiki. - Kuendesha miradi
ya kiuchumi. - Kuchukua mikopo na kurejesha. - Kuchangia mfuko wa jamii na bima
ya mikopo. - Kushiriki kikamilifu katika kuendesha miradi ya pamoja ya kikundi
Vikundi vya VICOBA huandaa mipango yao na kufanya maamuzi yote kwa njia ya
vikao ; ambavyo ni mkutano wa kila wiki , Mkutano Mkuu maalumu na Mkutano Mkuu
wa kawaida wa mwaka.
Kwa sasa vikundi
hivi huendesha shughuli zao chini ya sheria ya sekta isiyo rasmi na kuendesha
shughuli zake chini ya uangalizi/ ulezi wa serikali za mitaa au halmashauri za
miji na wilaya husika. Vikundi vinavyofadhiliwa na mashirika hulelewa na
kupatiwa msaada wa kitaalamu kupitia mashirika yao pamoja na ofisi za serikali
za maeneo yao wanayohusika. Ili kuhakikisha taratibu zao zinafuatwa kikamilifu
na wanachama wake ni muhimu vikundi kujitungia sheria ndogo ili kuthibiti
ukiukaji wa taratibu zilizowekwa na kuhakikisha kwamba kila mmoja anawajibika
ipasavyo.
Mafunzo ndio
shughuli inayopewa kipaumbele zaidi katika mfumo huu wa VICOBA. Hii ni kwa
sababu tafiti mbalimbali zilizofanyika zinaonyesha kuwa kukosekana kwa ujuzi au
mbinu za kibiashara ndio kiini cha matatizo yanayozorotosha jitihada za kuleta
maendeleo endelevu nchini hususani kwa wananchi waishio vijijini.
Mafunzo ya mfumo
wa VICOBA yamegawanyika katika makundi makubwa matatu ambayo ni:- (a) Mafunzo
ya uongozi wa kikundi na uendeshaji wa shughuli za kuweka na kukopa (b) Mafunzo
ya mbinu za biashara ya kuchagua, kupanga na kusimamia mradi wa ki-uchumi
(c) Mafunzo ya teknolojia rahisi za kuboresha ujuzi wa uzalishaji wa bidhaa za
wana-kikundi kama vile ufugaji wa nyuki, (Bee keeping) kilimo bora cha
mbogamboga kazi za mikono, ufugaji kuku, mbuzi ng’ombe, kuuza mayai, kuchimba
kisima cha maji, biashara ya usafirishaji,n.k Mafunzo haya hutolewa kabla ya
wanachama wa kikundi kuchukua mkopo. Lengo la mafunzo haya ni kuwaandaa
wana-kikundi kiujuzi na kuwawezesha, kubuni, miradi mizuri ya kiuchumi na
kuandaa mipango ya namna nzuri ya kuendesha na kusimamia biashara hizo. Mafunzo
ya Kuweka na Kukopa na yale ya mbinu za biashara hutolewa kwa kipindi 12 kila
wiki wanakikundi hufundishwa kipindi kimoja. Wakati huu wa mafunzo pia huweka
akiba zao kwa njia ya hisa ili kutunisha mfuko wao ambao baadaye hutumika kwa
kukopeshana. Mafunzo ya teknolojia rahisi hutolewa kwa wana-kikundi
wanaoiendesha miradi ya uzalishaji bidhaa mbalimbali kama vile kazi za mikono,
ufugaji, kilimo cha mbogamboga na shughuli zingine zinazohitaji ubunifu na
mafunzo maalumu. Mafunzo haya hutolewa ili kuongeza ubora wa bidhaa
zinazozalishwa Uchangiaji wa gharama za mafunzo Kwa kawaida wanachama wa VICOBA
hufundishwa mafunzo wanayotaka wao wenyewe. Vikundi vimeanzishiwa mfuko wa
mafunzo ambao kila mwanachama huchangia kiasi kidogo cha fedha kwa ajili ya
kuchangia gharama za mafunzo haya. Kutokana na uwezo mdogo wa wanavikundi,
wafadhili mbalimbali ikiwemo Serikali na Mashirika yasiyo ya kiserikali
yamekuwa yakijitokeza kuchangia gharama ya mafunzo haya. Mfano Mashirika ya
CARE Tanzania, WCRP, WCST, WWF, Ofisi ya Makamu wa Rais, WWF Tanzania, ITECO
Engineering, Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe, Uropean Union, shirika lisilo
la kiserikali la LAMP, Orgut, FREBU CO. LTD, nk
Kulingana sheria mama za mfumo huu wa VICOBA, mwanachama anatakiwa
kuweka hisa 1-3 kila wiki. Kiwango cha hisa huamuliwa na wanakikundi wenyewe.
Hata hivyo, kulingana na thamani ya fedha yetu kiwango cha chini kinachoweza
kumnufaisha mwanachama kwa sasa ni shilingi mia tano (500). Mwanachama
anaruhusiwa kuweka hisa moja, mbili hadi tatu kila wiki ili kutunisha mfuko.
Matumizi ya Hisa ya mwanachama Hisa ni muhimu zana kwa mwanachma kwa sababu
zifuatazo: (i) Ni akiba ya mwanachama ambayo huichukua mwishoni mwa mzunguko
pamoja na faida au wakati mwingine wowote apatapo matatizo kulingana sheria za
kikundi chao. Kwa kawaida hisa zinazochukuliwa katikati ya mzunguko hutolewa
bila faida (ii) Hisa hutumika kama kigezo cha kujua kiwango cha mkopo ambacho
mwanachama wa kikundi anaweza kuomba kutoka
kwenye benki yao.
Mfumo wa VICOBA unamruhusu mwanachama kuchukua mkopo hadi mara tatu ya hisa
alizoweka. Hata hivyo, uamuzi wa kupatiwa mkopo huo utazingatia matumizi na
uhakika wa mwanachama kumudu kurejesha kwa wakati unaotakiwa. (iii) Hisa
hutumika kama dhamana ya mkopo unaotolewa kwa mwanachama wa kikundi kidogo cha
watu watano. Dhamana ya awali ni ya mkopaji mwenyewe (Primary Guarantor) na
dhamana ya pili ni ya wanachama wenzake wanne (4) wa kikundi kidogo (Secondary
Guarantors) Hii inamaanisha kuwa ili kuhakikisha kuwa mikopo yote inayotolewa
kwa wanachama 5 wa kikundi kidogo inadhaminiwa kikamilifu mambo yafuatayo
yanatakiwa kuzingatiwa: (a) Wanachama wa kikundi kidogo wasiruhusiwe kuchukua
mkopo wakati mmoja. Tofauti ya mwezi mmoja hadi miezi miwilli ni kipindi kizuri
kwa wastani wa watu wawili wawili kila awamu (b) Kunatakiwa pawepo na
makubaliano maalumu baina ya mwanachama anayekopa na wale wanaomdhamini juu ya
hatua zinazoweza kuchukuliwa na wadhamini endapo mdhaminiwa hatatimiza wajibu
wa kulipa deni lake kwa uzembe (c) Mwanachama anayekopa kutoka kwenye benki ya
kikundi anatakiwa kuchangia mfuko wa bima ya majanga itakayokubaliwa na kikundi
kwa mfano kufariki kwa mkopaji, kuugua kwa muda mrefu na kupoteza uwezo wa
kufanya kazi/ kulemaa kwa mkopaji kuunguliwa au kuibiwa mali za biashara ya
mkopaji, ukame, nk Taratibu za utoaji na urejeshaji wa mikopo. Mikopo
inayotolewa kwa wanachama wa VICOBA unatakiwa kurejeshwa na nyongeza (Interest)
ndogo ambayo hutumika kwa kutunisha mfuko wa kikundi. Nyongeza hii hugawanywa kama
faida kwa wanachama kwa kuzingatia kiwango cha hisa alizoweka kila mmoja.
Mikopo ya mwanzo ambayo kwa kawaida huwa midogo kuliko mikopo inayofuata
hutakiwa kulipwa kwa kipindi cha miezi 3 . Lengo ni kumwezesha mkopaji aweze
kulipa haraka na kuchukua mkopo mkubwa pale hisa zake zinavyopanda ambao
utamwezesha kumudu kuanzisha na kuendesha biashara madhubuti zaidi Mfumo wa
VICOBA unamtaka mkopaji kurejesha mkopo aliokopa mwishoni mwa kipindi cha mkopo
wake kwa awamu moja. Mkopaji anatakiwa kulipa sehemu ya nyongeza inayoiva kila
ifikapo wiki ya mwisho ya mwezi. Sehemu ya mwisho hulipwa pamoja na mkopo
Mfano: Endapo mwanachama atakapokopeshwa shilingi 100, 000.00 kwa nyongeza ya
10% (10,000.00) kwa kipindi cha miezi mitatu atarejesha kama ifuatavyo:- Mwezi
wa 1 Mwezi wa 2 Mwezi wa 3 Jumla 3,400 3,300 3,300 100,000 110,000 Endapo mkopo
wa thamani hiyo hiyo (Shilingi 100,000.00) utarejeshwa kwa kipindi cha miezi
sita kwa gharama (nyongeza) ya asilimia ishirini 20% (20,000.00), marejesho
yatakuwa kama ifuatavyo:- Mwezi wa 1 Mwezi wa 2 Mwezi wa 3 Mwezi wa 4 Mwezi wa
5 Mwezi wa 6 Jumla 3,400 3,400 3,300 3,300 3,300 3,300 100,000 120,000 Kwa
kawaida mwanachama anayemaliza kurejesha mkopo wake vizuri anaruhhusiwa kuomba
mkopo mwingine mara moja ili kufidia pengo la mtaji katika biashara yake.
Ufuatiliaji na Uthibiti wa shughuli za vikundi vya VICOBA Makatibu wa vikundi
vya VICOBA wanatakiwa kufuatilia mwenendo wa vikundi vyao na kuandaa taarifa za
kila mwezi, miezi mitatu na taarifa za kila mwaka ambazo hujadiliwa na
kupitishwa na mikutano mikuu ya vikundi vyao. Afisa (Mkufunzi) anatakiwa kutoa
maelekezo na msaada wa kiufundi pale inapobidi na kuwajulisha wafadhali wa
vikundi na wadau wengine juu ya maendeleo ya vikundi kadiri inavyotakiwa.